Walimu wapya Missenyi walipwa zaidi ya mil.24

Sunday, March 10, 2013 | comments



Walimu wapya Missenyi walipwa zaidi ya mil.24
Na. Fredrick Laizer, Missenyi
ZAIDI ya sh milioni 24  zimelipwa  kwa walimu wapya 99 wakiwamo wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.
Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari Wilayani hapa, Joachiam Njiani, alibainisha hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake na kusema kuwa fedha hizo zimelipwa kwa walimu hao  waliopangiwa katika shule mbalimbali kuanzia Machi mwaka huu.
Alisema kati ya fedha hizo, walimu wa sekondari wamelipwa sh milioni 15,540,000 na walimu wa shule za msingi wamelipwa sh milioni 9,450,000.
Aidha, alisema walimu hao wamelipwa kwa utaratibu uliopangwa na serikali kwa mwalimu wa daraja la tatu “A” atalipwa sh 30,000 kwa siku saba, mwalimu wa stashada atalipwa sh 30,000 kwa siku saba na mwalimu wa shahada atalipwa sh 45,000 kwa siku saba na kuongeza kuwa malipo hayo ni tofauti na nauli.
Alisema halmashauri ilitarajia kupata walimu 73 wa shule za Sekondari,ambapo walimu wenye Shahada ni 52 na Stashahada ni 21  lakini walioripoti mpaka sasa  ni walimu 56 wakiwemo walimu wenye Shahada 36 na Stashahada 20.
Njiani  alisema walimu hao wapya watapelekwa kwenye shule zenye upungufu mkubwa wa walimu hasa maeneo ya vijijini.
Aidha kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Wilayani hapa Bw. Alfred Maijo alibainisha kwa upande wa shule za msingi walimu wapya walioripoti mpaka sasa ni walimu 43 kati ya walimu 45 waliokuwa wamepangwa mwaka huu.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi ina jumla ya walimu 802 huku mahitaji halisi yakiwa ni walimu 981 katika shule 95  za msingi zenye wanafunzi 38,214 .
Alisema walimu hao wapya watapelekwa kwenye shule zenye upungufu mkubwa wa walimu hasa maeneo ya vijijini ambako kuna uhaba wa walimu kulingana na idadi ya wanafunzi alisema Maijo’’
Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. MISSENYI DISTRICT COUNCIL - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger