Baraza la Madiwani lapitisha bajeti ya bilioni 21

Tuesday, March 5, 2013 | comments

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi.Elizabeth S. Kitundu akifafanua jambo wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kujadili bajeti ya 2013/2014


Baraza la Madiwani lapitisha bajeti ya bilioni 21
Na Fredrick Laizer
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, limepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya zaidi ya sh. bilioni 21 kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Mpango wa bajeti hiyo ulipitishwa na baraza la madiwani katika mkutano maalumu na iliwasilishwa na Ofisa Mipango wa Halmashauri hii, Issaya Mbenje kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji.
Bajeti hiyo iliyopita bila kupingwa ilikuwa ni sh. bilioni 21,322,665,939 ikiwa ni ongezeko la sh. bilioni 2,998,139,526 sawa na ongezeko la asilimia 14.1 ya bajeti iliyopita ya mwaka wa fedha wa 2012/2013, ambayo ilikuwa sh. bilioni 18,324,526,413.
Mbenje alisema kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele mbalimbali ikiwamo kukamilisha miradi ambayo haikukamilika kwa miaka ya nyuma.
Pia kuhimiza kilimo cha umwagiliaji, kuimarisha utawala bora na ushiriki wa jamii katika kupanga na kutekeleza miradi pamoja na kuwa na soko la ki-mkakati eneo la Mutukula mpakani na nchi ya Uganda ili kupanua wigo wa biashara ya mazao na bidhaa nyingine ndani na nje ya nchi.
Alisema bajeti ya mwaka 2013/14 kiasi cha sh. 12,223,019,500 ni kwa ajili ya mishahara, sh. 6,192,078,439 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na sh. 2,907,568,000 ni matumizi mengineyo.
Ofisa huyo alisema kuwa kiasi cha sh. 1,500,000,000 kinatarajiwa kuchangiwa na wananchi.
Mkutano huo wa madiwani ulikuwa chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, William Katunzi, ambapo bajeti hiyo ilionesha ina mpango wa kukusanya sh. 1,128,173,000 kutokana na mapato ya ndani pekee kwa mwaka 2013/2014.
“Naomba madiwani kufuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao ili iwe na ubora na thamani ya fedha inayotumika,” alisema Katunzi.
Aliwataka watendaji wa ngazi zote kufanya kazi kwa kujituma na kuzingatia uadilifu pamoja na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa lengo la kuleta tija ndani ya halmashauri.

Share this article :

Post a Comment

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. MISSENYI DISTRICT COUNCIL - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger