Friday, March 29, 2013 | comments

KAMATI YA FEDHA YAFANYA UKAGUZI WA MIRADI MBALIMBALI YA HALMASHAURI
Kamati ya Fedha,Utawala na Mipango Wilayani hapa imefanya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi
Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe.Wiliam Katunzi(katikati) akipewa maelekezo na Mhandisi wa Umwagiliaji wakati wa ukaguzi wa mradi wa umwagiliaji Kyakakera   
Kaimu Afisa Mipango(W) Missenyi Bw.Deus Joseph (katikati) akiwaonesha  moja ya darasa la Shule ya Msingi Kashaba Wajumbe wa Kamati ya Fedha walipokuwa katika ukaguzi wa miradi hivi karibuni

Moja ya mifereji ya mradi wa umwagiliaji katika Skimu ya Kyakakera iliyopo kata ya Kyaka  

Walimu wapya Missenyi walipwa zaidi ya mil.24

Sunday, March 10, 2013 | comments



Walimu wapya Missenyi walipwa zaidi ya mil.24
Na. Fredrick Laizer, Missenyi
ZAIDI ya sh milioni 24  zimelipwa  kwa walimu wapya 99 wakiwamo wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera.
Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari Wilayani hapa, Joachiam Njiani, alibainisha hayo alipozungumza na mwandishi wa habari hii ofisini kwake na kusema kuwa fedha hizo zimelipwa kwa walimu hao  waliopangiwa katika shule mbalimbali kuanzia Machi mwaka huu.
Alisema kati ya fedha hizo, walimu wa sekondari wamelipwa sh milioni 15,540,000 na walimu wa shule za msingi wamelipwa sh milioni 9,450,000.
Aidha, alisema walimu hao wamelipwa kwa utaratibu uliopangwa na serikali kwa mwalimu wa daraja la tatu “A” atalipwa sh 30,000 kwa siku saba, mwalimu wa stashada atalipwa sh 30,000 kwa siku saba na mwalimu wa shahada atalipwa sh 45,000 kwa siku saba na kuongeza kuwa malipo hayo ni tofauti na nauli.
Alisema halmashauri ilitarajia kupata walimu 73 wa shule za Sekondari,ambapo walimu wenye Shahada ni 52 na Stashahada ni 21  lakini walioripoti mpaka sasa  ni walimu 56 wakiwemo walimu wenye Shahada 36 na Stashahada 20.
Njiani  alisema walimu hao wapya watapelekwa kwenye shule zenye upungufu mkubwa wa walimu hasa maeneo ya vijijini.
Aidha kwa upande wake Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Msingi Wilayani hapa Bw. Alfred Maijo alibainisha kwa upande wa shule za msingi walimu wapya walioripoti mpaka sasa ni walimu 43 kati ya walimu 45 waliokuwa wamepangwa mwaka huu.
Alisema Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi ina jumla ya walimu 802 huku mahitaji halisi yakiwa ni walimu 981 katika shule 95  za msingi zenye wanafunzi 38,214 .
Alisema walimu hao wapya watapelekwa kwenye shule zenye upungufu mkubwa wa walimu hasa maeneo ya vijijini ambako kuna uhaba wa walimu kulingana na idadi ya wanafunzi alisema Maijo’’

Baraza la Madiwani lapitisha bajeti ya bilioni 21

Tuesday, March 5, 2013 | comments

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi.Elizabeth S. Kitundu akifafanua jambo wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kujadili bajeti ya 2013/2014


Baraza la Madiwani lapitisha bajeti ya bilioni 21
Na Fredrick Laizer
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, limepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya zaidi ya sh. bilioni 21 kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Mpango wa bajeti hiyo ulipitishwa na baraza la madiwani katika mkutano maalumu na iliwasilishwa na Ofisa Mipango wa Halmashauri hii, Issaya Mbenje kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji.
Bajeti hiyo iliyopita bila kupingwa ilikuwa ni sh. bilioni 21,322,665,939 ikiwa ni ongezeko la sh. bilioni 2,998,139,526 sawa na ongezeko la asilimia 14.1 ya bajeti iliyopita ya mwaka wa fedha wa 2012/2013, ambayo ilikuwa sh. bilioni 18,324,526,413.
Mbenje alisema kuwa bajeti hiyo imezingatia vipaumbele mbalimbali ikiwamo kukamilisha miradi ambayo haikukamilika kwa miaka ya nyuma.
Pia kuhimiza kilimo cha umwagiliaji, kuimarisha utawala bora na ushiriki wa jamii katika kupanga na kutekeleza miradi pamoja na kuwa na soko la ki-mkakati eneo la Mutukula mpakani na nchi ya Uganda ili kupanua wigo wa biashara ya mazao na bidhaa nyingine ndani na nje ya nchi.
Alisema bajeti ya mwaka 2013/14 kiasi cha sh. 12,223,019,500 ni kwa ajili ya mishahara, sh. 6,192,078,439 kwa ajili ya miradi ya maendeleo na sh. 2,907,568,000 ni matumizi mengineyo.
Ofisa huyo alisema kuwa kiasi cha sh. 1,500,000,000 kinatarajiwa kuchangiwa na wananchi.
Mkutano huo wa madiwani ulikuwa chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, William Katunzi, ambapo bajeti hiyo ilionesha ina mpango wa kukusanya sh. 1,128,173,000 kutokana na mapato ya ndani pekee kwa mwaka 2013/2014.
“Naomba madiwani kufuatilia kwa karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao ili iwe na ubora na thamani ya fedha inayotumika,” alisema Katunzi.
Aliwataka watendaji wa ngazi zote kufanya kazi kwa kujituma na kuzingatia uadilifu pamoja na uwajibikaji katika matumizi ya fedha za umma na kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa lengo la kuleta tija ndani ya halmashauri.

 
Support : Creating Website | Johny Template | Mas Template
Copyright © 2011. MISSENYI DISTRICT COUNCIL - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Mas Template
Proudly powered by Blogger