|
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bi.Elizabeth S. Kitundu akifafanua jambo wakati wa Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani la kujadili bajeti ya 2013/2014 |
Baraza la Madiwani lapitisha bajeti ya bilioni 21
Na Fredrick Laizer
BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya
Wilaya ya Missenyi, limepitisha makadirio ya mapato na matumizi ya zaidi ya sh.
bilioni 21 kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.
Mpango wa bajeti hiyo ulipitishwa na
baraza la madiwani katika mkutano maalumu na iliwasilishwa na Ofisa Mipango wa
Halmashauri hii, Issaya Mbenje kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji.
Bajeti hiyo iliyopita bila kupingwa
ilikuwa ni sh. bilioni 21,322,665,939 ikiwa ni ongezeko la sh. bilioni
2,998,139,526 sawa na ongezeko la asilimia 14.1 ya bajeti iliyopita ya mwaka wa
fedha wa 2012/2013, ambayo ilikuwa sh. bilioni 18,324,526,413.
Mbenje alisema kuwa bajeti hiyo
imezingatia vipaumbele mbalimbali ikiwamo kukamilisha miradi ambayo
haikukamilika kwa miaka ya nyuma.
Pia kuhimiza kilimo cha umwagiliaji,
kuimarisha utawala bora na ushiriki wa jamii katika kupanga na kutekeleza miradi
pamoja na kuwa na soko la ki-mkakati eneo la Mutukula mpakani na nchi ya Uganda
ili kupanua wigo wa biashara ya mazao na bidhaa nyingine ndani na nje ya nchi.
Alisema bajeti ya mwaka 2013/14
kiasi cha sh. 12,223,019,500 ni kwa ajili ya mishahara, sh. 6,192,078,439 kwa
ajili ya miradi ya maendeleo na sh. 2,907,568,000 ni matumizi mengineyo.
Ofisa huyo alisema kuwa kiasi cha
sh. 1,500,000,000 kinatarajiwa kuchangiwa na wananchi.
Mkutano huo wa madiwani ulikuwa
chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, William Katunzi, ambapo bajeti hiyo
ilionesha ina mpango wa kukusanya sh. 1,128,173,000 kutokana na mapato ya ndani
pekee kwa mwaka 2013/2014.
“Naomba madiwani kufuatilia kwa
karibu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika kata zao ili iwe na ubora na
thamani ya fedha inayotumika,” alisema Katunzi.
Aliwataka watendaji wa ngazi zote
kufanya kazi kwa kujituma na kuzingatia uadilifu pamoja na uwajibikaji katika
matumizi ya fedha za umma na kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi
washiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kwa lengo la kuleta tija
ndani ya halmashauri.